Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Ruvuma
WAZIRI wa Kilimo, Mhe Prof. Adolf Mkenda ameagiza utaratibu wa ununuzi wa mahindi uzingatiwe huku akionyesha kuridhishwa na namna zoezi hilo linavyoendeleshwa katika mkoa wa Ruvuma ambao wananchi wameonyesha kuridhika.

Hayo ameyasema jana tarehe 22 Septemba 2021 katika Hamashauri ya Wilaya ya Peramiho, Mbinga na Songea wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Ruvuma kujionea namna zoezi hilo linavyoendelea husuani kwenye mikoa iliyotangazwa awali kuanza kununuliwa kwa zao hilo.

“Watu wana matarajio makubwa kwamba serikali itanunua mahindi lakini kiasi chenyewe hatukutangaza kununua yote maana lengo la serikali lilikuwa kuchangamsha soko na malengo makubwa ilikuwa kumsaidia mkulima mdogo”

“Kwahiyo niliona baada ya ziara ya Mtwara tulikubaliana na Naibu  Waziri kwamba tutawanyike kuangalia hali inavyokwenda mimi nikasema nije Ruvuma maana ndio inazalisha mahindi kuliko mkoa mwingine wowote.” Amekaririwa Mhe Mkenda

Amebainisha kuwa walipofika mkoani hapo walisimama kuangalia zoezi hilo linavyokwenda na matokeo yameonyesha kuwa wananchi wameridhika na utaratibu uliopo wa ununuzi wa mahindi.

“Kwa kiasi hicho napenda kuipongeza NFRA na kwa sababu hawakunifahamu mimi ni nani wakati naingia hata mkuu wa kituo hakuniona nilizungumza na wakulima wanaouza wamesema utaratibu unaenda vizuri”

“Lakini wamesema kuna changamoto ya magunia ambayo NFRA wameshaifanyia kazi hivyo isitokee kisingizio kuwa mahindi yameshindwa kuuzika kwa ajili ya hilo,” Amesema Waziri Mkenda

Amesema tayari bei ya NFRA kununua mahindi imeshatangazwa kuwa ni kaisi cha Tsh 500 lakini inaweza kutokea watu wakaacha kuuza kwa kusubiri bei ipande ambapo alieleza haiwezekani kununuliwa yote.

“Mtu mwenye mahindi mengi asafirishe kwenda kuuza kwenye masoko makubwa ili kuondoa changamoto kwa ambao mahindi yao hayajanunuliwa, ili ziwepo takwimu za watu ambao mahindi yao wamenunuliwa kwa bei iliyopangwa na serikali,” Amesema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema wakulima wapo kidogo lakini ni wafanyabiashara zaidi hivyo kama mkoa wapo pamoja kutoruhusu suala la ununuzi wa mahindi kugeuka sokomoko badala ya tija ambayo Rais amedhamiria.

“Nilitoa maekezo na nayarudia kituo cha Ruhiko ambacho ndio makao makuu ya mkoa huu cha NFRA kitumike kama kituo cha kupokelea mahindi kulingana na uwepo na maghala na manunuzi yasimame”

“Kama mtu anaweza kuleta gari kubwa (Semi Trailler) lenye tani zaidi ya 30 huyo siyo mkulima ni mfanyabiashara, kama ni mkulima nitataka kujua shamba alilolimia lipo wapi maana ni mkulima mkubwa na taarifa hizo ambazo mkuu wa wilaya atakuwa na taarifa za kila mkulima,” Amesema.

Amewataka wakulima waliopo kwenye orodha iliyotolewa apewe taarifa za shamba lilipo vinginevyo ajiengue ili apeleke mahindi kwenye masoko makubwa na si kubanana, na wakulima wadogo waachwe ili mazao yao yanunuliwe.