Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo ametangaza kuyafuta madaraka ya waziri mkuu Mohamed Hussein Roble,katika kile kinachoonekana kuwa ni kuongezeka kwa mvutano mkali baina ya viongozi hao ambao umeitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro mpya.
Rais Abdullahi kupitia taarifa yake iliyotolewa alhamisi amesema waziri mkuu amekiuka katiba ya mpito na kwa hivyo madaraka yake makubwa ya kiutendaji yamefutwa.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kwamba,madaraka ya waziri mkuu yaliyoondolewa ni pamoja na uwezo wake wa kuwafuta kazi na kuwateua maafisa wa serikali, hadi pale uchaguzi utakapomalizika nchini humo.
Wiki iliyopita, Roble alimtuhumu rais Farmajo kuwa na nia ya kumpokonya mamlaka juu ya masuala ya uchaguzi na usalama na kuyalimbikiza mikononi mwake.