RAIS wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma ambaye alihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela baada ya kukaidi agizo la Mahakama kuhusu kesi ya rushwa dhidi yake, ameruhusiwa kumaliza kifungo chake akiwa nyumbani kutokana na kuumwa kwake.

Idara ya Magereza imetangaza msamaha huo wa kiafya miezi miwili tu tangu Zuma (79) aanze kutumikia kifungo hicho ambapo amelazwa katika hospitali moja nje ya Mahakama hiyo tangu Agosti 6 kwa maradhi ambayo hayajafahamika.

Idara hiyo ilisema rais huyo wa zamani anayetumikia kifungo jela alifanyiwa upasuaji mwezi uliopita na kwamba hawawezi kufichua kile anachosumbuliwa nacho lakini anaweza tu kuthibitisha kuwa walipokea ripoti zaidi ya moja ya matibabu.

Agosti 14, Zuma alifanyiwa upasuaji ambao hadi sasa haijaelezwa ulikua wa nini ila Idara ya Magereza imesema kwamba uamuzi huu mpya ulitokana na ripoti ya kiafya waliyopata kuhusu Zuma, hata hivyo wamesema atahitajika kufuata masharti atakayopewa na watamfuatilia kuhakikisha anamaliza kifungo chake.

Hii inakuja karibu miezi miwili baada ya rais wa zamani kuanza kutumikia kifungo chake cha miezi 15 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kuidharau na Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini. Zuma atatumikia kifungo kilichobaki nyumbani