Serikali imeandaa kitini ambacho kitatoa mwongozo wa jinsi mashirika yasiyo ya kiserikali yatakavyonufaika na misamaha ya kodi iliyopo kwa mujibu wa sheria.

Rais Samia ameyasema hayo leo Septemba 30, 2021 jijini Dodoma wakati wa mkutano mkuu wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (Nacongo) uliozikutanisha NGOs zote zinazofanya kazi hapa nchini.

Rais Samia ametoa kauli hiyo baada ya Mwenyekiti wa Nacongo, Dk Lilian Badi awali akiwasilisha risala yao alisema  NGOs zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa misamaha ya kodi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, upatikanaji wa vibali vya kazi kwa raia wasio wakitanzania.

 “Changamoto hizi zikifanyiwa kazi zitasaidia mashirika yasiyo ya kiserikali kuweza kuchangia maendeleo kwa taifa kwa kushirikiana na serikali,” amesema Dk  Liliani.

Aidha akizungumzia suala hilo, Rais Samia alisema “naandaa kitini ambacho kitatoa mwongozo wa namna mashirika yasiyo ya kiserikali yatakavyonufaika na msamaha wa kodi ambayo baadhi yao wanastahili kupata.

 “Tunafahamu kwamba kuna changamoto katika mifumo yetu ya kodi na pia zipo baadhi ya taasisi ambazo zinastahili kupata mikopo. Tumeanza kufanyia kazi masuala yote haya.

Alisema kuhusu changamoto ya upatikanaji wa vibali tayari serikali imeweka mfumo wa kielektroniki ambao umepunguza urasimu na vibali vinapatikana haraka ndani ya siku moja hadi tatu tofauti na ilivyokuwa zamani.

Kuhusu ucheleweshaji wa utoaji wa vibali vya utekelezaji wa miradi na afua mbalimbali, Rais Samia amesema; “natoa rai kwa mamlaka za serikali za mitaa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ili kwa pamoja tujenge nchi yetu.”