Wakuu wa mikoa yote nchini wameagizwa kuhakikisha wanawasimamia vizuri Wafanyabiashara wadogo (Wamachinga) ikiwa ni pamoja na kuwatengea maeneo ambayo hayatakuwa na bughudha kwao na kwa wengine.

  Agizo hilo limetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu Chamwino  mkoani Dodoma, wakati wa hafla ya kuwaapisha Mawaziri wanne pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

 Ameagiza ni lazima Viongozi hao wa mikoa waandae mipango mizuri itakayowawezesha Wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao kwa mpangilio na si kama hali ilivyo sasa.

  Hata hivyo Rais Samia Suluhu Hassan ametaka jambo hilo lifanyike bila ya kutumia nguvu na bila ya kumuonea mtu.

  Kwa upande wa Wafanyabiashara hao wadogo , Rais Samia Suluhu Hassan amewataka kufuata sheria zilizopo  wakati wanapofanya shughuli zao.

  Rais Samia Suluhu Hassan amesema amelazimika kutoa kauli hiyo baada ya kuona katika maeneo mengi Wafanyabiashara  hao wamekuwa wakifanya kazi hata katika maeneo yasiyostahili na kuleta usumbufu kwa watu wengine, hali ambayo pia imekuwa ikiikosesha Serikali mapato.