Rais wa  Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Sudan ya Kusini Salva Kiir Mayardit, Balozi Albino Ayuel Aboug, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Balozi Aboug amesema ujumbe huo pamoja na mambo mengine, Rais Salva Kiir Mayardit ametaka kuimarishwa zaidi kwa uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na Sudan Kusini.

Amesema Sudan Kusini inaomba kutumia Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo yake na pia kununua  chakula kutoka Tanzania.

Aidha, Balozi Aboug amesema Sudan Kusini pindi Reli ya Kisasa (SGR) itakapokamilika ingependa kusafirishia bidhaa zake kupitia reli hiyo.

Pia, amesema Sudan Kusini bado inahitaji kupata walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili kuanzia ngazi ya shule za msingi kutoka nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Rais Samia amemuhakikishia mjumbe huyo kuwa Tanzania iko tayari kuendeleza ushirikiano na uhusiano uliopo kwa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili kwa manufaa ya pande zote mbili.

Kuhusu ombi la kutumia Bandari ya Dar es Salaam, Mhe. Rais Samia amemuhakikishia mjumbe huyo kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Sudan Kusini kutumia Bandari ya Dar es Salaam katika kukuza uchumi wa nchi zote mbili.