Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis Jumapili ameihimiza Hungary "kumkumbatia kila mtu," kauli yake ikionekana kumlenga Waziri Mkuu Viktor Orban. 

Papa Francis alikutana na Orban, ambaye sera zake za uhamiaji zinakinzana na wito wa kiongozi huyo wa kidini anayeunga mkono ujumuishaji na kuwakaribisha wahamiaji wanaotafuta maisha bora Ulaya. 

Kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani mwenye umri wa miaka 84 anayefanya ziara ya siku nne Ulaya ya kati, alikaa mjini Budapest kwa masaa saba pekee kabla ya kuelekea nchi jirani ya Slovakia. 

Vatican na maafisa wa Hungary wamesisitiza kuwa Papa Francis hajaidharau Hungary kwa kukaa muda mchache nchini humo, na kwamba serikali ya Hungary ilimualika kwa ajili ya ibada maalum ya kutoa shukrani. 

Orban amejitokeza wazi kuwa mtetezi wa tamaduni za Kikristo barani Ulaya ambazo haziingiliana na tamaduni za wahamiaji ambao wengi wao wanatokea katika mataifa ya kiislamu.