Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, amewatolea wito waumini kutoa kipaumbele kwa wahanga wa matendo ya unyanyasaji unaofanywa na baadhi ya makasisi badala ya kuwa na hofu juu ya hadhi na sifa ya kanisa. 

Kupitia ujumbe wa video alioutoa, Papa Francis amesema kanisa linaweza kunusurika iwapo litakuwa tayari kukubali ukweli kuhusu matendo hayo ya kikatili na kutafuta msamaha kwa njia za kiungwana kutoka kwa walioathirika. 

Kiongozi huyo amesema anafahamu kwamba kukiri makosa ni jambo la kufadhaisha, lakini amesisitiza ni muhimu ili kupata msamaha wa kweli na kufungua njia mpya ya kueneza upendo. 

Ujumbe huo wa Papa Francis uliandaliwa kwa ajili ya mkutano wa kimataifa wa kuwalinda watoto unaofanyika nchini Poland unaohudhuriwa na wawakilishi wa kanisa pamoja na wataalamu wengine kutoka mataifa 20 duniani.