Mwili wa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji – William Ole Nasha unatarajiwa kuagwa Kiserikali kesho katika viwanja vya bunge jijini Dodoma.

Akitoa taarifa ya taratibu za mazishi ya Ole Nasha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema baada ya kuagwa mwili wa marehemu utasafirishwa kuelekea kijijini kwao Osinoni – Ngorongoro mkoani Arusha kwa ajili ya mazishi.

“Kesho siku ya Alhamisi tutafanya buriani ya kitaifa itakayohusisha viongozi wote katika viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania majira ya saa 5 asubuhi.

“Kwa sasa tunaendelea na vikao vya ndani kati ya Ofisi ya Bunge na sehemu alikokuwa anaabudu marehemu kiimani ili kuona namna tutakavyompa heshima ya mwisho,” amesema Mhagama.

Aidha, ameeleza kuwa baada ya mazungumzo yote marehemu Ole Nasha atapewa heshima za mwisho kisha kuanza safari ya kuelekea kijijini kwake Arusha ambako atapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele siku ya Jumamosi.

Naibu Waziri Ole Nasha alifariki dunia usiku wa tarehe 27 mwezi huu, nyumbani kwake mkoani Dodoma.