Mwenyekiti wa AU ataka Afrika iwe na kiti cha uanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la UN
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambaye ni mwenyekiti sasa wa Umoja wa Afrika AU amewasilisha malalamiko kadhaa ya bara la Africa katika mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ulioanza juzi mjini New York, likiwemo la bara la Afrika kupatiwa uanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la UN.
Tshisekedi ambaye ni kiongozi wa kwanza wa nchi za Afrika kuhutubia mkutano wa mwaka huu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambao katika ngazi ya juu ya viongozi wa nchi wanachama ulifunguliwa rasmi juzi, Tshisekedi, amezungumzia Afrika, kwa kuthibitisha mahitaji ya uwakilishi bora wa bara la Afrika kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Mwenyekiti wa AU ameomba nchi mbili za ziada zijumuishwe kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kundi la nchi wanachama wasio wa kudumu wa baraza hilo; na sambaba na hilo, nchi zingine mbili za Afrika zishiriki kwenye Baraza la Usalama kama wanachama wa kudumu walio na kura ya veto.
Katika hotuba yake hiyo kwa viongozi wanachama wa Umoja wa Mataifa, Rais wa Kongo DR amezungumzia pia vita vya kimataifa dhidi ya ugaidi na akasema: "Afrika imekataa kuwa hifadhi ya ugaidi wa kimataifa".
Mwenyekiti huyo wa mzunguko wa AU, amekosoa uwepo wa makundi yenye misimamo mikali, ambayo amesema yameenea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, baada ya kuenea nchini Mali, Niger, Nigeria, Cameroon, Chad, Burkina Faso na Msumbij.