Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry amemfuta kazi mwendesha mashtaka mkuu aliyekuwa anataka kumfungulia mashtaka kama mshukiwa katika mauaji ya Rais Jovenel Moise. 

Hatua hiyo imeitumbukiza Haiti katika mzozo mpya wa kisiasa. Waziri Mkuu Henry, ambaye ni daktari wa upasuaji aliteuliwa na marehemu Moise kama waziri mkuu siku chache kabla ya kuuwawa kwake na anataka kuleta maelewano kati ya mirengo mbalimbali ya kisiasa. 

Ila madai ya kuhusika kwake katika mauaji ya Moise, sasa yameifunika hiyo azma yake. Wiki iliyopita, mwendesha mashtaka katika kesi hiyo Bedford Claude alisema, rekodi za simu zinaonyesha kwamba mtu anayeshukiwa kuwa mpangaji mkuu wa mauaji ya Moise, aliwasiliana na Waziri Mkuu Henry usiku ambao uhalifu huo ulifanyika. 

Mshukiwa huyo ambaye alikuwa afisa katika wizara ya sheria na ambaye Henry amekuwa akimtetea, anadaiwa kutoroka na hajulikani alipo kwa sasa.