Samirah Yusuph.
Maswa. Masule Cosmas (05) amefariki dunia  baada ya kujeruhiwa na fisi wakati akiwa machungani na wenzake na baadhi ya viungo vyake kuliwa na mnyama huyo.

Kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu Richard Abwao amewaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo limetokea jana Augost 09, 2021 katika kijiji cha Mwamang'ori wilaya ya Maswa mkoani hapa.

Kamanda Abwao amesema kuwa mtoto huyo alikuwa na wenzake wawili wakiwa wanachunga ng'ombe na mbuzi katika mashamba ambayo yapo mbali kidogo na makazi yao.

"Fisi huyo alitokea kwenye kichaka na kuanza kuwakimbiza na alifanikiwa kumkamata na kuanza kula baadhi ya viungo vya mwili, ambavyo ni shavu la kulia, na kumtoa ngozi yote ya kichwa na macho yote mawili".

Abwao amesema kuwa wananchi walimtafuta fisi huyo na na baada ya kumpata walimuua, mwili wanmtoto huyo umefanyiwa uchunguzi na daktari na baadae kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

Aidha jeshi la polisi limetoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa watoto wao dhidi ya wanyama wakali.

Mwisho.