Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema ofisi yake inafanya jitihada za kuwa na mkutano wa wadau wa siasa siku chache zijazo ili kujadili na kuondoa mvutano kati ya vyama vya siasa na jeshi la polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari, leo Jumatatu tarehe 6 Septemba, jijini Dar es Salaam, Jaji Mutungi alisema, Polisi ndio wanaosimamia mikutano ya vyama vya siasa, kwa maana ya kutoa ulinzi, hivyo ametaka kiongozi huyo na wale wa vyama kukutana, ili kukubaliana namna bora ya kutelekeza jambo hilo.

Amesema, tayari amekutana na IGP Sirro na kukubaliana kuwapo kwa mkutano huo, ambao hata hivyo, hakueleza utafanyika lini.

"Imekuwa kila mkutano vya vyama vya siasa tunaona askari wamejazana, this is not a military state,Tumeliona hilo, tukasema tuwaite wadau tujadili. Sitarajii kuona vyama vya siasa vikiendelea na hiyo mikutano yao wakati jitihada hizi zinafanyika," amesema Jaji Mutungi akisisitiza vyama vya siasa kuwa na subira.

Amesema katika mkutano huo, wanataka kuondoa kitu ambacho polisi wanadhani vyama vya siasa vinakosea na kile ambacho vyama vya siasa vinadhani polisi wanakosea.