Mfanyabiashara na muwekezaji wa Simba SC Mo Dewji leo ametangaza rasmi kujiuzulu nafasi yake uenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ndani ya Simba SC na nafasi yake itachukuliwa na aliyekuwa makamu wake Salim Abdallah (Try Again).
Akizungumza katika video ambayo ameipost kupitia akaunti yake ya Instagram, Mo Dewji ameanza kwa kusema;
“Asalam akeikum, Bwana Asifiwe, naomba kutoa taarifa yangu kwa wanachama na mashabiki wa Simba. Kwanza nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa wana-Simba, mmetuunga mkono kwa miaka minne kama mwenyekiti wa bodi. Ninatoa shukrani zangu kwenu nyote kwani bila nyinyi, mashabiki, wapenzi na wanachama wa Simba tusingezeza kufika hapa.
“Napenda nichukue fursa hii kuwashukuru viongozi wote wa Simba Sc na Wajumbe wa Bodi kwa kunipa ushirikiano mkubwa, kwenye uongozi wangu kwa miaka minne. Kwenye hii miaka minne tumepata mafanikio makubwa, tumechukua mataji manne ya ligi na tumefika hatua nzuri kwenye Champions League.
“Muda umefika mimi kama Mohammed Dewji, tumefanya mkutano tarehe 21, 2021 na tumekubaliana kwamba mimi nitaachia ngazi kuwa Mwenyekiti wa Simba Sc. Ninaomba sana wana-Simba msifikirie kwamba mimi nimeondoka kwenye Simba, mimi bado nipo Simba na bado ni mwekezaji wa Simba, naipenda Simba na nitaendelea kuipenda Simba mpaka siku yangu ya mwisho.
“Tumekubaliana kwamba kwa sababu mimi muda mwingi nakuwa nje ya nchi, ninasafiri sana, tunahitaji kuwa na mwenyekiti ambaye muda mwingi yupo, atakayeiongoza klabu na uwepo wake ni muhimu sana. Nilikuwa na makamu wangu, Salim Abdallah Muhene ‘Try Again’ ambapo tuna makubaliano kati yangu mimi nay eye pamoja na Bodi.
“Natumia fursa hii kumteua Salim ‘Try Again’ kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Simba Sc. Salim ana uzoefu mkubwa wa kuiongoza Simba, huko nyuma amewahi kufanya kazi vizuri sana tukishirkiana kuijenga Simba. Namtakia kila la heri katika kuiongoza Simba, tutashirikiana nae katika kila jambo.
“Akitaka mwongozo wangu mimi nipo tayari kushirikiana naye. Mungu amtangulie Salim na viongozi wote wa Simba. Mimi bado nipo, nitajihusisha Zaidi na kusimamia maendeleo ya vijana kuijenga Simba Sc na bodi itashiriki kuijenga klabu.
“Ni Maisha tu, baada ya kupiga hatua kwenye uongozi unawaachia wengine wanaiendesha klabu. Asanteni sana wana-Simba, Simba Nguvu Moja.