Mjumbe Maalumu wa Marekani nchini Haiti amejiuzulu, ikiwa ni miezi miwili tu baada ya kuteuliwa, akilaani hatua ya utawala wa Biden kuwarejesha wahamiaji wa Haito kutoka mpaka wa Marekani na Mexico nchini kwao. 

Katika barua yake kali ya kujiuzulu, mjumbe huyo maalumu wa wizara ya mambo ya kigeni Daniel Foote, amesema hatohusishwa na uamuzi wa Marekani usiyo wa kiutu na haki, wa kuwafurusha wakimbizi wa Haiti na wahamiaji haramu kwenda nchini Haiti. 

Katika barua hiyo aliyoielekeza kwa waziri wa mambo ya nje Antony Blinken, Foote ameielezea Haiti kama eneo ambako wanadiplomasia wa Marekani wamefungiwa ili kulinda majengo kwa sababu ya hatari inayosababishwa na magenge yenye silaha yanayodhibiti maisha ya kila siku. 

Hatua ya kujiuzulu kwa Foote imekuja baada ya utawala wa rais Joe Biden kuanza wiki iliyopita, kuwapakia wahamiaji wa Haiti waliovuka na kuingia nchini humo kutokea Mexico, kwenye ndege na kuwarudisha nchini mwao.