Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kuna uwezekano mkubwa wa kutokea kwa ukame kutokana upungufu mvua unaotarajiwa kutokea katika kipindi cha mvua za vuli zinazotarajiwa kuanza kunyesha hivi karibuni.

Imebainishwa kuwa katika kipindi cha mvua za Oktoba hadi Desemba mikoa mingi itakuwa na upungufu mkubwa wa mvua ambazo zitakuwa chini ya wastani hadi wastani na pia kunatarajiwa kuwepo kwa vipindi vya joto kali lisilo la kawaida.

TMA imetoa tahadhari hiyo leo Septemba 2, 2021 wakati wa utabiri wa mvua za Vuli, ambazo ni mahsusi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini zinazotarajiwa kuanza kwa kusuasua katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba 2021 ikiwa na mtawanyiko na muendelezo usioridhisha katika maeneo mengi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa TMA, Dk. Hamza Kabelwa amesema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha mvua za Vuli zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani na zinatarajiwa kuambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi yanayopata mvua za Vuli.

Amesema hali hii itapekeleka kutokea kwa athari mbali mbali zitakazotokana na hali ya ukavu kwa maeneo yatakayokosa mvua ikiwemo upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi na kutokeza kwa magonjwa ya mlipuko, kutokana na upungufu wa maji safi na salama.

Athari zingine ni uwezekano wa kujitokeza upungufu wa malisho na maji hivyo kusababisha kujitokeza kwa migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Uwezekano wa kutokea matukio ya moto katika mapori na misitu, hivyo mamlaka husika zinashauriwa kupanga mikakati mahsusi ya kukabiliana na hali hiyo.

Amesema, msimu wa mvua za Vuli ni mahsusi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro na Pwani ya kaskazini, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Dar es Salaam na Tanga, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Katika ukanda wa Ziwa Victoria, Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma wilaya za Kibondo na Kakonko.

"Kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na inavyotarajiwa katika kipindi chote cha msimu kwa ujumla mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka" amesema Kabelwa.

Amesema, baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.

Aidha Mamlaka TMA, imetoa ushauri katika sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo,usalama wa Chakula ,Mifugo na Uvuvi,Utalii na Wanyamapori,Usafiri na Usafirishaji,Nishati ,Maji na Madini,Mamlaka za Mji,Sekta ya Afya ,Sekta binafsi pamoja na Menejimenti za Maafa kuhakikisha zinachukua tahadhari za mapema ili kuweza kuepukana na majanga yoyote yanayoweza kujitokeza katika kipindi huu hicho cha mvua chache.

Pia wameshauriwa kuendelea kufuatilia utabiri unaotolewa na wataalamu mbalimbali kipindi chote cha Mvua za Vuli.

Credit:Jamiiforums