Majaliwa: Vipaji Vya Vijana Kimichezo Vitaendelezwa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewahakikishia wadau na wapenzi wa michezo nchini kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika tasnia hiyo ili kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana.
Amesema uwekezaji huo utawawezesha vijana kushindana katika masoko ya michezo ya ndani na nje ya nchi, hivyo kuimarisha ajira, mapato yatokanayo na michezo na kuinua mchango wa sekta ya michezo katika pato la Taifa.
Waziri Mkuu ametoa taarifa hiyo jana (Ijumaa, Septemba 10, 2021) wakati wa kuahirisha Mkutano wa Nne wa Bunge la 12 jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi tarehe 2 Novemba, 2021.
“Nyote mtakubaliana nami kwamba kumekuwepo na mwamko mkubwa wa masuala ya sanaa, burudani na michezo nchini. Hivi sasa, michezo imekuwa chanzo kikubwa cha biashara, utalii, kuimarisha afya na ajira kwa vijana wetu.”
Waziri Mkuu amesema kwa kuzingatia hilo, Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi za kukuza michezo nchini. Hatua hizo ni pamoja na kuundwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Michezo na kurejesha mashindano ya UMITASHUMTA, UMISSETA na SHIMIWI.
Hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Michezo nchini na kukubali kudhamini mashindano ya wanawake ya CECAFA ili kutoa motisha kwa wanawake kushiriki zaidi katika michezo.
Amesema mbali na kuziandaa timu, pia mfuko huo utatumika kuimarisha miundombinu ya michezo na upatikanaji wa vifaa vya michezo, kuendeleza na kuwezesha shule na vituo vya umahiri wa michezo, kuendesha programu za mafunzo ili kupata wataalamu wa kutosha, kuwezesha programu za michezo kwa jamii na mashindano ya Kitaifa na Kimataifa.
Mheshimiwa Majaliwa amesema mfuko huo pia utasaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuziandaa vyema timu za Taifa za michezo mbalimbali na kuziwezesha kushiriki kwa tija katika mashindano na michezo ya kimataifa.
Pia, Waziri Mkuu ameipongeza timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu (Taifa Stars) kufuatia ushindi wa mabao matatu kwa mawili dhidi ya Madagascar katika hatua ya pili ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar.
“Aidha, tunazitakia heri timu ya wanawake ya kriketi inayoshiriki mashindano ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia nchini Botswana, timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) itakayoshiriki mashindano ya COSAFA nchini Afrika Kusini, timu ya mchezo wa wavu inayoendelea kushiriki mashindano ya Afrika nchini Rwanda.”
“Ninavitakia kila la heri pia vilabu vyetu vya Azam, Biashara United, Simba na Yanga katika uwakilishi wao kwenye michuano ya Shirikisho na Ligi ya Mabingwa ya Chama cha Soka barani Afrika (CAF).”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Rais Wallace Karia kwa usimamizi mzuri wa soka nchini.
Kuhusu suala la uendeshaji wa vilabu vya soka nchini, Waziri Mkuu amewapongeza wawekezaji na watendaji wa vilabu vya Azam, Simba na Yanga kwa uwekezaji mkubwa na usimamizi mzuri wa vilabu hivyo kwenye soka ambao umeanza kuzaa matunda.
“Nitumie nafasi hii pia kukipongeza kituo cha matangazo cha Azam (Azam Media) hususan upande wa matangazo ya runinga kwa kuuibua na kuutangaza vyema mchezo wa masumbwi nchini. Juhudi hizo za Azam Media wakishirikiana na wadau wengine zimewezesha wanamasumbwi wetu kutumia vizuri fursa hiyo kukuza vipaji vyao.”
Waziri Mkuu pia amempongeza bondia Twaha Kiduku kwa kumtwanga Dulla Mbabe katika pambano lililovuta hisia za Watanzania wengi. “Vilevile, nimpongeze bondia Hassan Mwakinyo kwa kumdunda mpinzani wake Mnamibia Julius Indongo kwa TKO na kutetea mkanda wake wa Chama cha Ngumi Afrika (ABU).”
Waziri Mkuu amesema wanamasumbwi hao wameendelea kuifanya Tanzania itambulike zaidi ulimwenguini.