Mahakama Kuu yatupilia mbali kesi ya Kikatiba ya Freeman Mbowe
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali kesi ya kikatiba ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe aliyokuwa akilalamika kwamba haki zake za kikatiba zilikiukwa wakati wa kumkamata, kumweka kizuizini na hatimaye kumfungulia kesi akikabiliwa na mashtaka ya ugaidi.
Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo mbele ya Jaji John Mgeta baada ya kukubaliana na hoja moja kati ya tatu za Serikali ya pingamizi la awali kuwa maombi hayo hayako sawa kisheria kwasababu yanapingana na kifungu 4(5) na kifungu cha 8(2) cha sheria ya haki za msingi na utekelezaji wa majukumu sura ya tatu.
Kwamba Mbowe ana njia nyingine za kupata hayo anayo walalamikia.
Jaji alisema, wakati maombi hayo yameletwa, wakati huo huo kuna mwenendo wa kesi katika Mahakama nyingine ambako Mbowe anashtakiwa kesi ambayo ndiyo msingi wa malalamiko hayo.
Jaji Mgeta alisema Mbowe anatakiwa kuwasilisha malalamiko yake katika Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Uhujumu Uchumi ambako ndio sehemu sahihi kwani ndiko kesi yake ya msingi inasikilizwa.
Mbowe alifungua kesi hiyo ya kikatiba Julai 30 mwaka huu , mahakamani hapo dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika kesi hiyo namba 21 ya mwaka 2021, Mbowe anapinga utaratubu uliotumika kumkamata, kumweka kizuizini na hatimaye kumfungulia kesi ya uhujumu uchumi akikabiliwa na mashtaka ya ugaidi.