Mkuu wa kikosi maalum cha jeshi kilichompindua Rais Alpha Conde amesema maafisa wa serikali ya Guinea sasa hawatoruhusiwa kusafiri nje ya nchi. Kanali Mamady Doumbouya pia amesema marufuku ya kutotoka nje katika maeneo yaliyo na migodi, imeondolewa. 

Kanali Doumbouya amekiambia kikao cha mawaziri wa Conde akiwemo waziri mkuu na maafisa wengine wakuu serikalini kwamba warudishe pia magari yao rasmi. 

Mapinduzi hayo katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi iliyo na utajiri mkubwa wa madini ya bauxite ambayo yanatumika kutengeneza chuma cha pua, yamesababisha bei ya chuma hicho kuongezeka na kufikia bei ambayo haijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka kumi. Vikosi vingine vya jeshi la Guinea bado havijatoa tamko kuhusu mapinduzi hayo yaliyofanyika jana.