Korea Kusini imefanikiwa kurusha kombora la masafa marefu kutoka kwenye nyambizi ya kijeshi na kuwa taifa la saba duniani kumiliki teknolojia hiyo mamboleo inayotishia kuongeza uhasama na jirani yake Korea Kaskazini. 

Jaribio hilo la leo ni mafanikio makubwa kwa Korea Kusini ambayo imekuwa ikijiimarisha kijeshi kukabiliana na kitisho kutoka Korea Kaskazini iliyo chini ya vikwazo vya kimataifa vinavyoipiga marufuku kuunda silaha nzito ikiwemo zile za nyuklia. 

Ikulu ya Korea Kusini imesema jaribio la leo ambalo limeshuhudiwa na rais Moon Jae-in limehusisha ufyetuaji wa kombora kutoka nyambizi mpya ya kijeshi ya Ahn Chang-ho na kufanikiwa kuifikia shabaha mamia ya kilometa. 

Jaribio la Korea Kusini limefanyika saa chache baada ya Korea Kaskazini kufyetua makombora mawili ya masafa marefu yaliyoelekezwa kwenye bahari ya mashariki inayofahamika pia kama bahari ya Japan.