Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un ametangaza kurudisha laini za mawasiliano ya simu na Korea Kusini mwanzoni mwa mwezi ujao wa Oktoba. 

Shirika la habari la Korea Kusini, Yonhap limelinukuu shirika la habari la Korea Kaskazini, KCNA likiripoti taarifa hizo. 

Kim amesema mawasiliano hayo yatarejeshwa kama sehemu ya juhudi za kuimarisha uhusiano na kuleta amani katika Rasi ya Korea. Kim ameitaka Korea Kusini kuachana na sera zake za uadui na undumilakuwili. 

Aidha, kiongozi huyo wa Korea Kaskazini amesema sera za uadui za Marekani na kitisho cha jeshi, bado hazijabadilika na kwamba pendekezo la Marekani la hivi karibuni la kufanya mazungumzo ni jaribio la kuuficha uadui huo. 

Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana leo kujadiliana kuhusu hali ya Korea Kaskazini. Mkutano huo unafanyika kwa ombi la Marekani, Uingereza na Ufaransa.