Masalia ya kimbunga Ida yamesababisha mvua kubwa kuwahi kunyesha katika majimbo ya New York, New Jersey na Pennsylvania ya mashariki mwa Marekani, ambayo imeleta mafuriko katika nyumba za watu na kuzifanya barabara kuonekana kama mito.
Watu wasiopungua tisa wamethibitika kuuawa katika majimbo ya New York na New Jersey, wanane kati yao wakifa maji ndani ya nyumba zao. Maafisa wa mji wa Philadelphia jimboni Pennsylvania pia wamezungumzia kutokea vifo, bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.
Mvua hizo zimenyesha hadi alfajir ya jana Alhamis, na tayari shughuli za uokozi zinaendelea, ikitarajiwa kuwa miili zaidi ya waliokufa itapatikana.
Rais Joe Biden alizungumza jana kuainisha aina ya msaada utakaotolewa na serikali kuu mjini Washington, huku akijiandaa kutembelea jimbo la Louisiana lililoathiriwa vibaya na kimbunga Ida. Katika jimbo hilo, watu zaidi ya milioni moja hawana huduma ya umeme kwa zaidi ya wiki moja sasa.