Jeshi La Polisi Lasema Upepelezi wa Awali Unaonyesha Hamza Mohammed Alikuwa Ni Gaidi
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Camillius Wambura amesema, uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi kuhusu Hamza Mohamed aliyewaua askari watatu wa Jeshi la Polisi na na mlinzi mmoja wa kampuni ya SGA kisha naye kuuawa, umebaini kwamba Hamza Mohamed alikuwa ni gaidi wa kujitoa mhanga.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Septemba 2, 2021, Wambura amesema uchunguzi uliofanywa na polisi umebaini kwamba Hamza alikuwa akiishi kisiri huku akiwa amegubikwa na viashiria vyote vya ugaidi na kwamba alikuwa akijifunza mambo ya kigaidi kupitia mitandao ya kijamii ambayo kwa kipindi kirefu amekuwa akifuatilia mitandao inayoonyesha matendo ya Al-Shabab na makundi kama ISIS.
Ameongeza kuwa taarifa zinazodai kwamba Hamza aliwashambulia askari hao kwa sababu walimdhulumu madini yake, si za kweli kwa sababu uchunguzi umebaini kwamba hakuwa na madini wala fedha na kwamba umiliki wake wa mgodi wa dhahabu Chunya, ulisimama kwa muda mrefu.