Viongozi wa juu wa jeshi la Marekani wamesema walimshauri Rais Joe Biden kutowaondoa wanajeshi wote nchini Afghanistan. 

Wakihojiwa mbele ya kamati ya bunge la Marekani inayohusika na masuala ya silaha, viongozi hao wamesema kuondoka kwa majeshi yake Afghanistan ni ''kushindwa kimkakati''. 

Mkuu wa Majeshi, Jenerali Mark Milley ameonya kuwa makundi ya kigaidi yanaweza kujiunda tena ndani ya miezi 12 na kuishambulia Marekani. 

Amesema alipendelea kuvibakiza vikosi kadhaa Afghanistan ili kuzuia kuanguka kwa serikali ya Kabul iliyokuwa inaungwa mkono na Marekani na kuzuia Taliban kuchukua madaraka. 

Milley amekataa kusema ushauri aliompa Biden wakati alipokuwa anafikiria kuviondoa vikosi hivyo. 

Jenerali Frank McKenzie, mkuu wa kamandi kuu iliyokuwa inasimamia majeshi ya Marekani nchini Afghanistan amesema alipendekeza wanajeshi 2,500 wabakizwe Afghanistan.

Credit:DW