Serikali imesema kuwa itakuwa na jumla ya mashahidi saba katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo namba 16/2021 ni Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Lingwenya.
Hayo yamesemwa leo Jumatano, tarehe 15 Septemba 2021 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando mbele ya Jaji Mustapha Siyani, wakati shauri hilo lilipoanza kusikilizwa.
Wakili Kidando amedai shahidi wa kwanza ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Arusha, Ramadhani Kingai, ambaye sasa ni Kamanda wa Jeshi la Polisi, Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Dar ea Salaam.
Shauri hilo linasikilizwa baada ya mawakili wa Mbowe na wenzake, wakiongozwa na Peter Kibatala, kuweka mapingamizi mawili dhidi ya maelezo ya mshtakiwa Adam Kasekwa.
Mapingamizi hayo yaliwekwa baada ya Kamanda Kingai hapo awali kutoa ushahidi wake dhidi ya kesi ya msingi, ambapo alidai alichukua maelezo ya Kasekwa kwa hiari yake.
Mbele ya mahakama hiyo, Kibatala alitoa hoja za mapingamizi hayo, ikiwemo iliyodai kwamba mshtakiwa huyo alichukuliwa maelezo nje ya muda, kinyume cha kifungu cha 50 (1) sehemu A na B pamoja na kifungu cha 51 na 52 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, vinavyoelekeza mtuhumiwa kuchukuliwa maelezo ndani ya saa nne baada ya kukamatwa.
Kibatala alidai kuwa, maelezo hayo ni kinyume cha sheria kwa madai, mshtakiwa huyo alikamatwa tarehe 5 Agosti 2020 mkoani Kilimanjaro na kuhojiwa tarehe 7 Agosti 2020, Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Katika hoja ya pili, Kibatala alidai mshtakiwa huyo alichukuliwa maelezo hayo baada ya kuteswa.
Kufuatia hoja hizo, Wakili Kibatala aliiomba mahakama hiyo mbele ya Jaji Siyani, ifanye shauri dogo ndani ya kesi hiyo, ili mapingamizi yao yatolewe uamuzi.
Nao Mawakili upande wa Jamhuri wakiongozwa na Kidando, walikubali shauri hilo dogo lisikilizwe.
Kufuatia hoja hizo, Jaji Siyani aliridhia ombi hilo na kuanza usikilizwaji wa shauri dogo, ili ipate ushahidi kama mshtakiwa aliteswa wakati anahojiwa