Iran imekubali kuwaruhusu wakaguzi wa kimataifa kuweka vifaa vya ufuatiliaji katika vituo vyake vya nyuklia na kuendelea kuchukua vidio na kukusanya taarifa juu ya shughuli zake. 

Tangazo hilo limetolewa na Mohammad Eslami ambaye anaongoza shirika la nishati ya Atomiki la Iran baada ya kufanya mkutano na Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia IAEA Rafael Grossi mjini Tehran. 

Tangazo hilo huenda likaipa muda zaidi Iran kuelekea kwa mkutano wa bodi ya IAEA wiki hii ambapo mataifa yenye nguvu duniani yameikosoa Iran kwa kutoonyesha ushirikiano na wakaguzi wa kimataifa. 

Tehran imezuia taarifa zake zote juu ya oparasheni kwenye vituo vyake vya nyuklia wakati mazungumzo juu ya kuunusuru mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 ya mjini Vienna yamekwama.