Na WAMJW-DOM
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amezindua magari ya kliniki tembezi ya kisasa nne, pikipiki 160, mashine 50 za ‘GeneXpert’ pamoja na mashine 179 za ECG zilizogharimu billioni 6.2 ambazo zitasaidia kupunguza idadi au kuondoa kabisa wagonjwa wasiofikiwa wanaougulia majumbani hapa nchini.

Dkt. Gwajima Amezindua Kliniki hizo jana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, huku uzinduzi huo ukihudhuriwa na baadhi ya viongozi ngazi ya Wizara, TAMISEMI na Mkoa lengo likiwa ni kuboresha huduma za matibabu ya ugonjwa wa TB na Ukoma ili kuutokomeza nchini.

“Jumla ya Bilioni 6.2 zimetumika kununua magari haya ya kliniki tembezi na vifaa vya kutolea huduma za afya. Kiasi hiki ni kikubwa, sina budi kuwapongeza watumishi wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma kwa kufanikisha zoezi hili.” Amesema Dkt. Gwajima.

Amesema, Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2020, Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa takribani135,000, huku kati ya hao waliofanikiwa kubainiwa na kuwekwa kwenye matibabu walikuwa 85,597 sawa na asilimia 63, na kusisitiza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 duniani zenye tatizo kubwa la Kifua Kikuu.

Aliendelea kusema kuwa, takribani watu 26,800 walifariki katika kipindi cha mwaka 2020 licha yajitihada zinazofanywa na Wizara katika kufikia malengo ya kutokomeza Kifua Kikuu nchini, bado nguvu ya ziada inahitajika ili kuweza kuwafikia na kuwaibua wagonjwa takribani 49,403 ambao hatukuweza kuwaibaini na bado wanaendelea kuambukiza ugonjwa huo katika jamii yetu.

“Takribani watu 26,800 walifariki katika kipindi cha mwaka 2020. Licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara katika kufikia malengo ya kutokomeza Kifua Kikuu nchini, bado tunahitaji nguvu ya ziada kuweza kuwafikia na kuwaibua wagonjwa takribani 49,403 ambao hatukuweza kuwaibaini na bado wanaendelea kuambukiza ugonjwa huo katika jamii yetu”.kuwafikia wagonjwa.

Hata hivyo, Dkt. Gwajima amebainisha kwamba Dhima ya Wizara yake ni kutokomeza kifua kikuu nchini kwa makundi maalum yanayotambulika katika ngazi ya jamii kwa ajili ya ushirikishwaji katika mapambano hayo.

“Dhima ya Wizara ni kutokomeza Kifua Kikuu nchini hivyo basi, Wizara imebuni mikakati mahususi kwa ajili ya kuifikia jamii ambapo inajumuisha, kutumia Kliniki tembezi kwa ajili ya huduma mkoba za uchunguzi na ugunduzi wa Kifua Kikuu, kuongeza wigo wa mtandao wa maabara kwa kutumia teknolojia ya mashine za GeneXpert pamoja na kuimarisha mfumo wa lojistiki katika uratibu na ufuatiliaji wa huduma hizo ngazi ya jamii na Halmashauri kwa kutumia pikipiki.

Vile vile Dkt Gwajima amesema, Kliniki tembezi pamoja na vifaa vinavyozinduliwa ni kielelezo cha utayari wa kufikia malengo ya kitaifa na kidunia huku akibainisha kuwa kliniki hizo zimefungwa vifaa maalumu kama X-ray za kidigitali na Mashine za GeneXpert teknolojia za kisasa ambazo zitaweza kuibua wagonjwa walioko katika maeneo ambayo huduma hizi hazipatikani.

“Teknolojia hii ya kisasa iliyowekwa haina budi kuleta matokeo chanya katika kuibua wagonjwa hasa katika maeneo ambayo huduma za uchunguzi na ugunduzi wa Kifua Kikuu hazipatikani” amesema Dkt Gwajima.

Aidha, Dkt. Gwajima ametoa rai kwa watumishi watakao endesha kliniki hizo kufanya kazi kwa weledi, kuzitunza na kuzijali kwani gharama iliyotumika ni kubwa na pia matengenezo yake ni ghari.

“Kliniki tembezi hizi zitagawanywa katika Hospitali za Kanda ikiwemo Bugando (Kanda ya Ziwa), Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma (Kanda ya Kati), Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (Kanda ya Nyanda za Juu Kusini) na Maabara Kuu ya Kifua Kikuu iliyopo Dar es salam (Kanda ya Mashariki) na usimamizi wake utaratibiwa na Hospitali hizo kwa kushirikiana na Wizara” Amesema.

Kwa upande wa pikipiki Dkt. Gwajima amesema matarajio yake ni kumaliza tatizo la waratibu kushindwa kutekeleza kikamilifu majukumu yao ya uratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma, ikiwemo usambazaji wa dawa na vifaa tiba na kusaidia uibuaji wa wagonjwa wa TB na Ukoma kwa kiwango kikubwa na vile vile itasaidia kipindi cha dharura kwa akina mama wajawazito wanaohitaji damu wakati wa uzazi.