Kampuni ya madawa ya Pfizer imesema kuwa chanjo zake za COVID-19 zinafanya kazi kwa watoto kuanzia miaka mitano hadi 11. 

Kampuni hiyo imesema itaomba idhini ya Marekani ili iweze kulipatia kundi hilo chanjo, hatua muhimu kuelekea kuanza kuwachanja watoto hao. 

Chanjo inayotengenezwa na Pfizer na mshirika wake wa Ujerumani, BionTech tayari inatolewa kwa watoto wenye miaka 12 na zaidi. 

Lakini kutokana na watoto kurejea shuleni na kuongezeka kwa maambukizi ya kirusi cha delta, kunasababisha maambukizi kuongezeka kwa watoto na wazazi wengi wanasubiri chanjo kwa ajili ya watoto wao wadogo. 

Wakati huo huo, India itaanza tena kusafirisha chanjo za virusi vya corona kuanzia mwezi ujao wa Oktoba, miezi mitano baada ya kusitisha zoezi hilo wakati ikipambana na wimbi baya la maambukizi. 

Kampuni ya madawa ya India, ilikuwa msafirishaji mkubwa wa chanjo kupitia mpango wa kimataifa wa COVAX wa kununua na kusambaza chanjo za bure kwa nchi maskini zaidi duniani.