SERIKALI ya Tanzania imetaja baadhi ya faida za Bunge kuridhia Azimio la kuanzisha eneo la mkataba huru la biashara Afrika kuwa ni pamoja na kupatikana kwa masoko mapya ya mazao ya kilimo na hivyo kuchochea uzalishaji wake.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Profesa Kitila Mkumbo ameyasema hayo leo Alhamis Septemba 9 2021 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha azimio hilo.
Mhe. Mkumbo metaja baadhi ya faida hizo kwa Tanzania ni pamoja na kuimarisha mnyororo wa thamani ya mazao ambayo mengi yanawahusisha wakulima wadogo.
“Kuongeza uzalishaji na ajira kwa wakulima na wadau wanaohusisha na mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo…Kupatikana na soko kubwa la bidhaa ,” amesema Mhe. Mkumbo.
Nyingine ni kuongezeka kwa uzalishaji kwa wakulima, ajira na thamani ya mazao ya kilimo.
Profesa Mkumbo ametaja faida nyingine ni kupatikana kwa soko kubwa la bidhaa na huduma lenye idadi ya watu takribani bilioni 1.2 ukilinganisha na idadi ya watu takribani milioni 522 katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Afrika Kusini mwa Afrika (SADC.)
Pia kuongezeka kwa tija na ubora kwa bidhaa na huduma za Tanzania kutokana na kuongezeka kwa ushindani na hivyo kupelekea kupungua kwa bei za bidhaa.