WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema muswada wa Bima ya Afya kwa wote utakapokamilika utakuwa ni mkombozi mkubwa kwa Watanzania kwani utakwendakufanikisha mkakati wa Serikali wa kuwapatia watanzania huduma bora za afya.

Amesema Serikali inaendelea kufanya maboresho makubwa ya ujenzi wa miundombinu ya afya, zikiwemo hospitali pamoja na vifaa tiba, hii ikiwa ni dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na zenye uhakika. 

“Serikali inaimarisha upatikanaji wa bidhaa za Afya nchini ikiwa ni pamoja na dawa, vifaa tiba na kuanzia mwezi Juni, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 31 kwa ajili ya kuhakikisha vifaa hivyo vinapatikana hivyo nataka niwahakikishie watanzania kuwa Serikali itaendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa na huduma bora za afya nchini” Alisema.

Waziri Mkuu Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Septemba 25, 2021) wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kushiriki mbio za hisani zilizoandaliwa na benki ya NMB

Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeanza ujenzi wa kiwanda kwa ajili ya uzalishaji wa ‘Gloves’ na dawa aina tano zikiwemo vidonge, ‘syrup’, ‘Capsules’, kwa lengo la kukidhi mahitaji ya nchi.

“Kiwanda hicho kitasaidia kuokoa shilingi bilioni 33 ikilinganishwa na shilingi bilioni 54 kwa mwaka ambazo zinatumika kununua bidhaa za afya sita zitakazozalishwa kiwandani hapo”

Aidha, Waziri Mkuu ametoa pongezi kwa benki ya NMB na CCBRT kwa pamoja na wadau wengine kwa namna wanavyounga mkono Serikali katika kuwahudumua kinamama wanaopata ugonjwa wa Fistula

Naye, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano wanawake zaidi ya elfu tano miatano wameshatibiwa ugonjwa wa fistula na asilimia kubwa wametibiwa katika Hospitali ya CCBRT.

“Hii inatokana na kampeni ya inayoendeshwa kati ya Serikali na wadau ambao kuna mabalozi zaidi ya 3000 nchi nzima kushughulikia wagonjwa wa fistula na kuwapeleka katika hospital zinazotoa huduma za fistula.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna amesema kuwa lengo la mbio hizo zilikuwa ni kukusanya fedha kwa ajili ya wanawake wanaosumbuliwa na ugonjwa wa fistula.

Zaipuna amesema kuwa, kupitia mbio hizo za hisani wamefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi milioni 400 ambao zitaweza kutoa matibabu kwa kinamama 100 wanaosumbuliwa na ugonjwa wa Fistula

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU