Jeshi la Polisi limewatunuku hati ya ujasiri askari 11 waliopambana katika tukio la mtu aliyefahamika kwa jina la Hamza Mohamed, kuwashambulia askari na kuwaua wanne katika makutano ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Tukio hilo lilitokea Agosti 25 mwaka huu ambapo Hamza aliwaua askari watatu na mlinzi wa kampuni ya SGA kabla ya yeye kuuliwa.

Akizungumza mara baada ya kuwatunuku askari hao leo Septemba 20 kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la polisi nchini, Simon Sirro, Kamanda Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema lilikuwa tukio kubwa ambalo kama lisingedhibitiwa haraka lingeweza kuleta madhara makubwa.

Amesema katika tukio hilo kulikuwa na askari wengi na wote walifanya kazi nzuri lakini hao 11 walifanya vizuri zaidi.

“Askari hawa (Waliopambana na Hamza) miongoni mwao walikuwa ni Askari 11, ambao kwa mamlaka za kisheria za uendeshaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP amewapa zawadi ya vyeti vya ujasiri na zawadi ya pesa kwa kadri alivyoona inafaa.

“Askari Polisi walipambana kuhakikisha kwamba madhara makubwa zaidi ya yale yaliyotokea hayatokei, nani ambaye hafahamu kama yule mhalifu angeondoka na zile silaha zilizokuwa na magazine 2 na risasi 60 na zingine alizokuwa nazo nini kingefanyika. "-Amesema