Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amempongeza mgombea wa ukansela wa chama cha Social Democratic, SPD Olaf Scholz kwa kushinda uchaguzi uliofanyika siku ya Jumapili. 

Taarifa iliyotolewa jana na ofisi ya Merkel imeeleza kuwa kansela huyo anayeondoka madarakani, aliwasiliana binafsi na Scholz waziri wake wa fedha, siku ya Jumatatu. 

Ofisi hiyo pia imesema Merkel na mawaziri wataendelea na majukumu yao hadi serikali mpya ya shirikisho itakapoundwa na kuchukua rasmi madaraka. 

Kansela Merkel ataendelea kutekeleza majukumu yake ikiwemo kufanya ziara za nje na kuhudhuria mikutano ya viongozi wa serikali wa nchi nyingine. 

Aidha, shirika la habari la Ufaransa, AFP limeripoti kuwa kiongozi wa CDU, Armin Laschet pia amempongeza Scholz.