Aliyekuwa rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amesema ananuia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya mjini Paris, iliyomkuta na hatia ya kupata fedha za kampeni kwa njia haramu. 

Kwa hatia hiyo, Sarkozy amepewa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja. Hata hivyo, kifungo hicho atakitumikia nyumbani kwake, kwa kuvishwa bangili ya kielekroniki itakayowawezesha maafisa wa gereza kujua wakati wote mahali alipo. 

Mahakama hiyo imesema wakati wa kampeni ya mwaka 2012, Sarkozy alikiuka ukomo wa viwango vya bajeti inayokubalika kwa shughuli hiyo. 

Aidha, mahakama hiyo imesema chama cha Sarkozy cha UMP ambacho kimebadilisha jina na kuitwa Republicans, kilijaribu hila ya kuficha uhalifu huo kwa kuandika stakabadhi za bandia. 

Katika uchaguzi huo Nicolas Sarkozy alishindwa na mgombea wa chama cha kisoshalisti, Francois Hollande. Inasemekana Sarkozy hakuubuni mfumo huo wa udanganyifu, lakini alizifumbia macho ishara za wazi zilizoonyesha kuwa ulikuwa ukitumiwa.