Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amezindua mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake na kuwataka watakaotekeleza mfumo huo kutogeuka kuwa Jeshi la Polisi na watoa hukumu kwa wananchi.

Mhe. Ndaki ametoa kauli hiyo (27.08.2021) jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi wa mfumo huo ili kuongeza tija na kuinua pato la taifa kupitia sekta ya mifugo.

Amesema mfumo huo ni rahisi na ushirikishwaji hivyo ni vyema wakaguzi kutogeuka kuwa Jeshi la Polisi na kuwasumbua wadau wa sekta ya mifungo.

“Utaratibu huu ni wa ushirikishwaji, sasa tunapokuwa huko kufanya ukaguzi kuhusiana na ubora na viwango tusijigeuze sisi kuwa polisi. Kwa nchi yetu mfumo huu ni rahisi na ambao umelenga kuzipatia taarifa wizara, taasisi na wadau wengine kuhusiana na ukaguzi, ubora na usalama wa mifugo pamoja na mazao yake.” Amesema Mhe. Ndaki

Ameongeza kuwa umuhimu wa mfumo huo ni kuhakikisha utekelezaji wa wajibu wa kulinda afya za walaji, mifugo na mazao yake kwa kusimamia sheria, kanuni na taratibu jambo ambalo litasaidia wafugaji kuzalisha mifugo kwa tija kwa kutumia pembejeo na huduma zilizosajiliwa na kutambuliwa kisheria.

Aidha ametoa rai kwa wakaguzi kutumia mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake kuhakikisha sheria, kanuni, taratibu za kusimamia na udhibiti wa ubora, usalama na viwango stahiki vinasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo.

Pia, ametumia fursa hiyo, kutoa wito kwa wataalam wa wizara, mamlaka za serikali za mitaa, taasisi na wadau waliopo kwenye vyama vya tasnia kuhakikisha wakaguzi, wazalishaji, watoa huduma kwenye mifugo wanazingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo ili kuhakikisha mlaji wa mifugo na mazao yake anaendelea kunufaika kiafya na kimaslahi kupitia maziwa, nyama na mayai na bidhaa nyingine.

Waziri Ndaki amewaomba wafugaji wote nchini kujenga utamaduni wa kutumia pembejeo na malighafi zenye ubora, usalama, viwango stahiki kutoka kwenye vyanzo vilivyosajiliwa kwenye uzalishaji wa mifugo.

“Hatua hii muhimu itasaidia upatikanaji wa bidhaa bora zinazozalishwa, kuchakatwa na kukaguliwa na wataalam wa mifugo hapa nchini.” Amefafanua Mhe. Ndaki

Awali, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Miugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, Bw. Amosy Zephania amesema wizara imeanzisha na kuboresha mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake ambao umejikita kwenye tasnia za kuku, maziwa, nyama, mayai, ngozi, malisho na rasilimali za vyakula vya mifugo.

Amebainisha kuwa mfumo huo umeanishwa kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kupitia mradi wa maboresho ya ufugaji kibiashara (L-MIRA) ambao umewezesha kufanyika mapitio ya sheria tatu za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama ya mwaka 2010, Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003 na Sheria ya Veterinari ya mwaka 2003 na kanuni 12.

Bw. Zephania amesema mfumo huo umelenga kuongeza ari na hamasa ya uwekezaji kwenye sekta ya mifugo kwa kutatua changamoto za ubora, usalama na viwango stahiki kwenye mifugo, mazao ya mifugo na pembejeo za mifugo.