Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dr.Dorothy Gwajima, ameagiza Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kumkamata na kumhoji Askofu wa Kanisa na Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuhusu tuhuma anazozitoa dhidi ya serikali juu ya chanjo ya corona.

Amesema, licha ya Askofu Gwajima ambaye ni Mbunge wa Kawe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Dar es Salaam, kuwa shemeji yake, lakini amechoshwa na vitendo vyake.

Waziri Gwajima ametoa agizo hilo leo Jumanne, tarehe 17 Agosti 2021 akiwa Kijiji cha Kyatunge Wilaya ya Butiama mkoani Mara.

Agizo hilo amelitoa kipindi ambacho Askofu Gwajima amekuwa akitumia siku za Jumapili kanisani kwake, Ubungo Dar es Salaam, kuzungumzia chanjo ya corona ambayo inaendelea kutolewa nchini akisema yeye, rafiki zake na familia anazoziongoza hawatochanjwa.

Askofu Gwajima anawatuhumu viongozi wa serikali kuhongwa ili kuruhusu kuingizwa nchini kwa chanjo hiyo. Pia amekuwa akipinga chanjo hiyo kwamba si salama.