Na. Angela Msimbira NJOMBE
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Ummy Mwalimu amebariki maamuzi ya Baraza la madiwani kuhusu ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Walaya ya Njombe kujengwa katika Kijiji Kidegembye Kata ya Kidegembye, Halmashauri ya wilaya Njombe, Mkoani Njombe.

Akiongea na Viongozi wa Mkoa wa Njombe, Wilaya, Baraza la Madiwani na Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Waziri Ummy amesema amebariki maamuzi hayo kufuatia mvutano wa muda mrefu uliokuwepo wa eneo la ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri hiyo ambao umedumu tangu mwaka 2019.

Waziri Ummy amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kuhakikisha ujenzi unaanza mara moja kwa kuwa fedha zaidi ya shilingi milioni 900 zimetolewa na Serikali hivyo kazi ya ujenzi iendelee bila kuchelwa.

Waziri Ummy amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Njombe kunaza taratibu za kuomba fedha shilingi bilioni moja ambazo zimetengwa na Serikali katika mwaka wa fedha 2021/22 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi.

Ameendelea kusema kuwa kwa sasa mjadala kuhusu ujenzi wa Makao Mkuu umefungwa kinachotakiwa ni kujenga mahusiano mazuri katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuwataka madiwani kusimamia ujenzi huo ili uweze kukamilika kwa wakati.

Amemuagiza Afisa Mipango Miji wa Halmashauri wa Wilaya kuhakikisha wanapanga mpango wa kabambe wa eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ili iwe kama “satellite City”

Vilevile amewaagiza Halmashauri hiyo kuhakikisha wanabuni mkakati utakaoifanya Hospitali ya Matembwe inafanyakazi ya kutoa huduma za afya kwa wananchi

Aidha amewataka baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kusimamia ukusanyaji ya mapato ya ndani ya Halmashauri na kuhakikisha yanatekeleza kutatua kero za wananchi na kuwataka wakuu wa Idara kuhakikisha wanatenga asilimia 40 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.