Na Atley Kuni – KAHAMA.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amelazimika kuigeuza Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga kuwa sehemu ya Shamba darasa kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kote nchini.

Hatua hiyo ya Waziri Ummy imewafikisha viongozi hao katika miradi ya uwezeshaji ya wananchi kiuchumi kwenye eneo la Chapulwa, lenye ukubwa wa hekari 2000 huku hekari 90 zikiwa zimetolewa kwa mwekezaji, na katika eneo la Zongomera lenye hekari 2100, Hekari 500 zimegawanywa kwa wajasiriamali ili waendeshe shughuli za kibiashara na ufundi.

Wakionekana kuguswa na hatua zilizochukuliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, yakuwawezesha wanachi kujikwamua kiuchumi, Wakuu hao wa Mikoa wameaahidi kutumia fursa ya maarifa waliyopokea kwaajili ya Mikoa yao.

Akiongea kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa wenzake, Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa John Mongella, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, amesema ziara hiyo imewafungua macho, hivyo watachukua hatua za haraka katika kufanikisha azma hiyo kwakuwawezesha wananchi kwenye maeneo yao.

“Mhe. Waziri, Mimi kwa niaba ya viongozi wenzangu hatuna lakusema kwa sasa, ila tumuahidi Mhe. Rais kwamba, tunakwenda kuishi viapo vyetu, moja ikiwa nikuhakikisha maarifa haya ambayo wenzetu wa Kahama tumevuna kwao, sisi tutakwenda kufanya vizuri zaidi” alisema Mongella.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adamu Malima, hakusita kuonesha hisia zake mbele ya Waziri Ummy na kutoa maelekezo kwa Katibu Tawala wa Mkoa huo, kuhakikisha manunuzi ya Jozi tatu za Masofa ambazo zilikuwa zimepangwa kununuliwa na Ofisi hiyo ya Mkuu wa Mkoa kwenye maeneo mengine, sasa manunuzi hayo yafanyike kwenye kampuni ya *Wahitime Furniture* ya Kahama Shinyanga ilioanzisha kiwanda cha Furniture katika eneo hilo la biashara ikiwa ni jitihada zakuunga Mkono shughuli hiyo inayofanywa na vijana wazalendo wa kitanzania.

Awali akitoa maelezo Mbele ya Waziri wa Nchi na Ujumbe wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Anderson Msumba, alisema wao kama Manispaa walikaa na kuamua kutoa Hekari 500 bure kwa wananchi, lakini mara baada ya Mradi kuanza, sasa Halmashauri inakusanya shilingi Milioni. 80 kila mwaka, fedha inayoingia kama sehemu ya mapato ya ndani.