Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrison ametetea mkakati wa taifa hilo wa kuzifunga shughuli za kawaida kama sehemu ya juhudi za kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona hadi angalau asilimia 70 ya watu wa nchi hiyo watakapopata chanjo ya virusi hivyo. 

Akizungumza kwenye mahojiano na shirika la utangazaji la taifa, Morrison amesema kufungwa kwa shughuli za kawaida ndiyo msingi wa mkakati wa taifa wa kudhibiti janga la Covid-19 na maisha ya kawaida yatarejea baada ya asilimia 70 ya watu wote kuchanjwa. 

Kiongozi huyo ametoa matamshi hayo siku moja baada ya polisi kuwakamata mamia ya watu waliokuwa wakiandamana kwenye miji ya Sydney, Melbourne, New South Wales na Victoria kupinga kufungwa kwa shughuli za umma. 

Hadi sasa ni asilimia 30 pekee ya watu wazima nchini Australia ndiyo wamechanjwa kikamilifu dhidi ya Covid-19 kutokana na kusuasua kwa kampeni ya utoaji chanjo iliyotatizwa na uhaba wa chanjo ya Pfizer.