SALVATORY NTANDU, KAHAMA
Katika jitihada za kukabiliana na tatizo la mimba na ndoa za utotoni kwa watoto wenye umri chini ya umri wa 18 mkoani Shinyanga serikali imesema itaanza kuchukua  hatua kali za kisheria kwa baadhi ya watendaji wa vijiji na kata zilizopo katika maeneo ya vijijini watakaobainika kusuluhisha kesi za watu wanaowapa mimba wanafunzi.

Kauli hiyo ilitolewa leo Katibu Tawala msaidizi wa serikali za mitaa mkoa wa Shinyanga, Alphonce Kasanyi wakati akizungumza na madiwani wa halmashauri ya Ushetu,baada ya kukithiri  kwa matukio ya baadhi ya watumishi wa serikali kusuluhisha kesi za watu wanaowapa mimba wanafunzi.

Alisema kuwa katika maeneo ya vijijini wanafunzi wamekuwa wakipewa mimba na wanaume lakini hakuna hatua za kisheria zinazochukuliwa kutokana na baadhi ya viongozi wa serikali kupokea rushwa na kuyafumbia macho matukio hayo.

“Vijijini rushwa imetawala watendaji wetu wamekuwa vinara wa kusuluhisha kesi za mimba za wanafunzi na watoto wenye umri chini ya miaka 18 kinyume na maelekezo ya serikali kuhusiana namna ya kukabiliana na watu wanaowapa mimba wanafunzi,”alisema Kasanyi.

Amefafanua kuwa endapo itabainika kuna tukio la mwanafunzi kupewa mimba katika vituo vyao vya kazi wataanza kuwawajibisha kwa mujibu wa sheria ili kudhibiti kuongezeka kwa matukio hayo kwenye jamii ambayo yanasababisha wanafunzi hao kukosa haki zao.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya Ushetu Gagi Lala alisema kuwa atahakikisha wanatekeleza agizo hilo ili kudhibiti tatizo la mimba katika shule za msingi na sekondari hususani katika maeneo ya vijijini ambapo bado kumeshamiri  matukio hayo.

“Niwaagize watendaji wetu msijiingize katika vitendo hivi vya rushwa,tuwakamate wahalifu wote wanaotekeleza matukio hayo ili watoto wa kike watimize ndoto katika elimu,”alisema Lala.

Nae Gabriela Kimaro diwani wa kata ya Ulowa alisema kuwa endapo sheria zianza kuchukuliwa kwa watu wanaowapa mimba wanafunzi matukio hayo yatapungua na kusababisha wengi wao kutumiza ndoto zao.

“Vijijini kuna waendesha bodaboda na wafanyabiashara wanaopenda kujihusisha na mapenzi na wanafunzi kama wakiwajibishwa watawaogopa na watoto wetu watabaki salama,”alisema Kimaro.

Kwa mujibu wa ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) mikoa inayoongoza kwa kiwango kikubwa cha mimba za utotoni  ni  Shinyanga unaongoza kwa asilimia 59, Tabora asilimia 58, Mara 55,Dodoma 51 na Lindi asilimia 48.

Mwisho.