Watu wasiopungua 110 wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa kufuatia miripuko miwili ya mabomu iliyotokea nje ya uwanja wa ndege wa Kabul nchini Afghanistan.

Hospitali ya kituo cha upasuaji wa dharura mjini Kabul imetangaza kuwa maiti 90 na makumi ya majeruhi wamefikishwa hospitalini hapo.

Taarifa ya awali iliyotolewa na afisa wa Taliban ilisema watu wasiopungua 13 walikuwa wameuawa katika miripuko hiyo.

Watoto wadogo ni miongoni mwa waliouawa katika miripuko hiyo ya mabomu iliyotokea kandokando ya uwanja wa ndege wa Kabul jana jioni.

Hili ni shambulizi kubwa la kwanza kutokea mjini Kabul tangu rais Ashraf Ghani aitoroke nchi na mji mkuu huo wa Afghanistan kudhibitiwa na kundi la Taliban mnamo tarehe 15 Agosti.


Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Pentago, John Kirby amesema, mripuko mmoja umetokea karibu na lango la Abbey la kuingilia uwanja wa ndege wa Kabul na mripuko wa pili umetokea jirani kabisa na hoteli ya Baron iliyopo karibu na uwanja huo.

Kwa mujibu wa Kirby, askari 13 wa Marekani ni miongoni mwa waliouawa katika mashambulio hayo ya jana.