Na Zuena Msuya Kagera,
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amesema watumiaji wa Umeme Waliobadilishiwa Tozo za kutoa huduma (TARIFF) kutoka kundi moja kwenda jingine pasipo wao kubadilisha matumizi halisi watoe taarifa katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ili kufanyiwa marekebisho ya tozo hizo.

Wakili Byabato alisema hayo wakati akifunga Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakulima nchini maarufu kama Nane Nane kwa Mkoa wa Kagera yaliofanyika katika Uwanja wa Kyakailabwa, wilayani Bukoba Mkoani humo, Agosti 8, 2021.

Aidha aliwataka TANESCO kuhakikisha wanarekebisha TARRIF kwa makundi yote ya watumiaji wa umeme kulingana na matumizi husika ili kuondoa malalamiko kwa wateja.

“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wateja wa umeme, kuhusu kubadilishiwa TARRIF katika matumizi ya Umeme, pasipo wateja hao kubalisha matumizi yao halisi, wateja wa namna hiyo wanapotoa taarifa TANESCO washughulikiwe haraka iwezekanavyo na warudishiwe katika TARRIF za matumizi yao halisi, na kama matumizi ya mteja yamezidi kiwango cha awali cha TARRIF afahamishwe, na elimu itolewe kuondoa mkanganyiko”, alisema Wakili Byabato.

Aidha alifafanua kuwa katika Kundi la Matumizi Madogo ya Nyumbani (D1), ambao linahusisha wateja wenye matumizi ya wastani wa Uniti 75 kwa mwezi watapaswa kulipa gharama ya shilingi 9150 na kwamba katika kundi hilo, mteja atatozwa bei ya juu zaidi kwa kila uniti itakayozidi 75 kwa mwezi.

Katika kundi la Matumizi ya Kawaida (T1),  linahujumuisha wateja wenye matumizi ya kawaida ya umeme hususani wa Majumbaji , Wafabiashara, Viwanda Vidogo, Taa za Barabarani pamoja na Mabango, matumizi hayo ya umeme ni wastani wa zaidi ya  Uniti 75 kwa miezi mitatu mfululizo.

Vilevile kwa kundi la Matumizi ya Juu ya Msongo(T2), wateja wa kundi hilo ni wale wenye matumizi ya kawaida ya wastani wa uniti 7500 kwa mwezi.

Na mwisho ni  Kundi la Matumizi ya Juu ya Msongo wa Kati( T 3) ambapo wateja wake huunganishwa kwenye msongo wa kati wa umeme na matumizi yao ni zaidi ya Uniti 500 na umeme hupimwa kwa kilovolti 11 na zaidi.

Katika hatua nyingine aliwaeleza Wakazi wa Mkoa wa Kagera kuwa Wizara ya Nishati  Kupitia TANESCO wataweka Umeme katika eneo la kibiasha la Mkoa lilipo katikati ya Wilaya ya Misenyi na Bukoba Vijijini ili eneo hilo lianze kutumiwa na wafanyabisha pamoja na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Kwa mantiki hiyo aliwataka wafanyabishara kuendelea kuwekeza zaidi vitega uchumi katika eneo hilo kwa kuwa kutakuwa na umeme wa uhakika.

Wakati huohuo aliwataka baadhi ya watumiaji wa TANESCO wasio waaminifu kuacha tabia ya kuomba rishwa kwa wateja ili waunganishiwe umeme kwa kuwaambia kuwa wajiongeze akieleza kuwa kauli hiyo ni kitendo cha kuomba rushwa kwa wateja.

Hali kadhalika aliwaeleza wakazi wa Kagera kuwa hivi karibuni maeneo yote ambayo hayajafikiwa na umeme yatafikiwa kwa kuwa tayari wakandarasi wako kazini kutekeleza kazi hiyo kwa gharama ya shilingi 27,000 tu.

Na aliwasisitiza kuwa endapo afisa yeyote kutoka TANESCO, au  mkandarasi atataka kupewa chochote ili kumuunganishia umeme mwananchi, au akamtaka mwananchi ajiongeze ilia pate umeme, mwananchi huyo atoe taarifa sehemu husika, na ikiwezekana ampige picha na kurekodi kwa ushahidi zaidi kwa kwakuwa kufanya hivyo ni kuomba rushwa.