Na. Hassan Mabuye, Mbeya
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amezitaka ofisi zote za Wilaya na Mikoa kuwa na Daftari maalumu la orodha ya migogoro ya ardhi ili kuitambua na kuitatafutia ufumbuzi wake kwa wakati.

Waziri Lukuvi ameyasema hayo alipokutana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Mbarali mkoa wa Mbeya mwishoni mwa wiki wakati wa kuzindua mpango wa maalumu wa kukopesha wananchi gharama ya kupanga, kupima na kupewa hati kwa kushirikiana na Bank ya NMB.

Lukuvi amesema, katika maeneo mengi nchini kumekuwa na migogoro inayoibuka kila mara hasa ya mipaka na haipatiwi ufumbuzi wa kudumu na mengine imekuwa ikiibuka kwa kushtukiza kwa kuwa utatuzi wake haukushirikisha wataalamu wa ardhi na haijawekewa mipango ya kuitatua.

“tunajua ipo migogoro ya ardhi inayosababishwa na mipaka ambayo imeanzishwa na mamlaka, ipo mipaka ya kijiji na kijiji mipaka ya wilaya na wilaya na ipo mipaka ya na hifadhi na mipaka ya utawala. Basi tuijue migogoro hii kuitafutia ufumbuzi na kuitatua” amesema Lukuvi.

Katika hatua nyingine Waziri Lukuvi amezitaka halmashauri za wilaya kusimamia sheria katika usimamizi wa ardhi kwa kuwa mamlaka za upangaji wa ardhi yetu kwa Tanzania ni halmashauri za wilaya na ndio wenye ardhi iwe ya mjini au ya vijijini.

Ameongeza kwa kusema kuwa, uvunjaji wa sharia za ardhi umekuwa ni mkubwa sana kwa maana watu wamekuwa wakijenga hovyohovyo bila vibali vya ujenzi. Maeneo mengi watu wamejenga mpaka kwenye vyanzo vya maji, wanajenga katika viwanja ambavyo havikupimwa, tena nyingine ni nyumba kubwa zinajengwa bila hata kupewa onyo.

“ninatoa maelekezo kwa wakurugenzi wote nchi nzima watowe barua kwa watendaji wa mitaa na vijiji kwamba moja ya majukumu yao ni kusimamia uendeshaji na usimazi wa ardhi kwenye mitaa na vijiji vyao” amesisitiza Lukuvi.

Amesema kuwa, barua hii itawawezesha kuzuia ujenzi holela, manyanyaso katika ardhi, uporaji na kusimamia ujenzi unaozingatia sharia. Jambo hili litawasaidia kupata watoa taarifa za ardhi (land Rengers) na kuweza kudhibiti uonevu na uvunjifu wa sheria za ardhi.

Aidha, waziri lukuvi amezionya halmashauri ambazo husababisha kero nyingi za fidia kwa kunyang'anya ardhi za watu bila kulipa fidia na kuanza kuweka miradi ya kupima viwanja na kuviuza ili kupata fedha kwa kuwa sasaivi wakurugenzi wengi wameishajua kwamba ardhi ni mali 

Amezitaka halmashauri zote kuondoa kero hii ya fidia kwa kutenda haki ya kuwalipa wananchi fidia stahiki na kwa wakati bila kuzalisha migogoro mipya ya ardhi.