Ugiriki inakumbwa na wimbi kubwa la joto kali ambalo halijashuhudiwa kwa karibu miongo miwili wakati inazidisha juhudi za kuzima moto uliozuka maeneo kadhaa ya nchi hiyo kutokana na kupanda kwa kiwango cha joto. 

Watabiri wa hali ya hewa wameonya leo kuwa kiwango cha joto kinaweza kupindukia nyuzi 47 za kipimo cha Celcius katika muda wa wiki moja inayokuja, na kuongeza uwezekano wa maeneo mengi zaidi kuwaka moto. 

Mapema jana serikali imetuma ndege na vifaa vingine kwenda maeneo mawili ya Peloponnese na kisiwa cha Rhodes kudhibiti moto ambao tayari umeunguza maelfu ya hekari za misonobari na mizaituni tangu ulipozuka mwisho mwa juma. 

Wimbi la joto kali kusini mwa Ulaya pia limesababisha moto nchini Uturuki, Uhispania na Italia na wataalamu wamesema athari za mabadiliko ya tabia nchi ndiyo zinachochea hali hiyo.