Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imelitangaza Jimbo la Konde huko Pemba kuwa wazi baada ya mbunge mteule, Sheha Mpemba Faki kutangaza kujiuzulu kabla ya kuapishwa na taratibu za kujaza nafasi hiyo zitatangazwa hivi karibuni.

Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dk Wilson Mahera imeeleza kuwa tume imepokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Agosti 2 ikitoa taarifa kuwa mbunge huyo mteule aliandika barua kwa chama chake kukitaarifu kuwa hayupo tayari kuwawakilisha wananchi wa Konde katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na changamoto za kifamilia.