Tanzania na India zimekubaliana kuweka msisitizo katika uwekezaji katika mnyororo wa uongezaji wa thamani wa madini,vito vya thamani pamoja na mazao mbalimbali ikiwemo korosho ili kuuza bidhaa badala ya kuendelea na utamaduni wa kusafirisha malighafi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ametoa msisitizo huo wakati akipokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa India hapa nchini Mhe. Binaya Srikanta Pradhan na kuongeza kuwa njia pekee kwa Tanzania kuongeza ajira na kupunguza umasikini ni kuwekeza katika mnyororo wa uongezaji wa thamani katika bidhaa za kilimo pamoja na madini.

Pia Balozi Mulamula amepokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Uholanzi hapa nchini Mhe. Weibe Jacob DE BOER ambaye ameeleza kufurahishwa na mahusiano ya kihistoria yaliyopo baina ya Nchi hizo mbili.

Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Misri hapa Nchini Mhe Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa ambapo viongozi hao wamezungumzia juu ya uwekezaji katika sekta ya uvuvi hususani uvuvi katika eneo la bahari lenye kina kirefu (deep sea fishing),viwanda vya nyama lakini pia katika sekta ya afya kwa kujenga hopitali kubwa Jijini Dodoma.

Pia Balozi Mulamula kwa nyakati tofauti amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Korea Kusini hapa Nchini Mhe. CHO tae –ick na kuzungumzia maeneo ya ushirikiano ikiwemo kuimarisha diplomasia,uwekezaji na biashara.