Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali inatekeleza kwa vitendo Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III: 2021/2022-2025/2026) na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kwa lengo la kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu wote.

Wizara ya Kilimo na Wizara zingine zinatekeleza sera mbalimbali ambazo zitaiwezesha Serikali kufikia malengo iliyojiwekea katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo pamoja na Dira za Maendeleo za Taifa kwa pande zote mbili za Muungano.

Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda (Mb) ameyasema hayo  tarehe 30 Agosti 2021 wakati akizindua ripoti ya Sensa ya Kilimo, Mifugo, na Uvuvi ya mwaka wa Kilimo 2019/2020 katika ukumbi wa hoteli ya Morena Jijini Dodoma.

Amesema kuwa Utekelezaji wa Sera yoyote unahitaji ushahidi wa kisayansi ambao utakuwa macho na masikio ya Serikali kupima utekelezaji, tathmini, na ufuatiliaji wa malengo ambayo serikali imejiwekea.

Waziri Mkenda amesema kuwa Takwimu bora zinazokidhi viwango vinavyokubalika ni msingi muhimu wa Serikali kujipima katika dhana nzima ya kujenga uchumi shindani na wa viwanda ambayo ni matamanio ya vjongozi wote waliopewa dhamana ya kuongoza nchi.

Waziri Mkenda amesema kuwa Mazao ya kilimo yanayozalishwa hapa nchini yanakidhi mahitaji ya chakula cha watu wote Tanzania wapatao takribani milioni 60 kwa asilimia 100, idadi inayotokana na matokeo ya idadi ya watu kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012. Uzalishaji wa mazao pia unatoa ziada kwa ajili ya kuuza nje na kulipatia Taifa fedha za kigeni.

Ameeleza kuwa Shughuli za Kilimo ambazo zinajumuisha mazao, mifugo, misitu na uvuvi zimeendelea kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Nchi katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa kujenga Uchumi Shindani na wa Viwanda.

Aidha, shughuli hizi za uchumi zimeendelea kutoa ajira kwa zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wote wenye uwezo wa kufanya kazi hususani kwa wale wanaoshi katika maeneo ya vijijini na wengi wao wakiwa wanawake na vijana.

Awali akizungumza katika hafla hiyo Mtwakimu Mkuu wa Serikali Dkt Albina Chuwa amesema kuwa Sensa hiyo ni ya tano na kabla yake zilifanyika Sensa nne yaani mwaka 1971/72; 1993/94 na 1994/95, 2002/03 na ya nne ni ya mwaka 2007/08.

Amesema kuwa Tanzania imekuwa ikiendesha Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kila baada ya takribani miaka 10. Takwimu za uchumi zilizopo zinaonesha mchango wa shughuli za kilimo katika Pato la Taifa umeongezeka hadi asilimia 26.9 mwaka 2020 ikilinganishwa na asilimia 26.6 mwaka 2019.

Kiwango cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi za sekta hii ambazo zinajumuisha kilimo cha mazao, mifugo, misitu na uvuvi zilikua kwa asilimia 4.9 mwaka 2020, ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.4 mwaka 2019.

Kwa upande wake muwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe Jabir Shekimweri amesema kuwa uzinduzi huo umekuja wakati muafaka kwani itasaidia Wizara na Taasisi mbalimbali katika kuongeza tija na uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini.

Amesema kuwa takwimu hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kwa wakulima nchini kuanzia wakati wa kuandaa mashamba, Upatikanaji wa mbegu bora na kwa wakati, wakati wa mavuno pamoja na kuunganisha masoko ya wakulima.