Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na watoa huduma katika sekta ya Afya nchini wameelekezwa kutimiza wajibu wao kitaaluma kwa kuelimisha umma wa Watanzania kuhusu umuhimu wa kupata Chanjo ya UVIKO 19 ili waweze kufanya maamuzi sahihi.

Agizo hilo limetolewa  leo Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis katika mkutano wake na waandishi wa Habari.

Mhe. Mwanaidi amesema miongoni mwa majukumu ya maafisa hao ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii katika masuala mbalimbali ikiwemo suala la chanjo dhidi ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Korona (UVIKO 19).

"Mtakumbuka kuwa, mnamo tarehe 28 Julai, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alizindua mpango wa chanjo ya UVIKO 19 Kitaifa kwa kuonesha njia na kuchanjwa dhidi ya ugonjwa huo, hivyo nampongeza Rais wetu kwa hatua hiyo muhimu ya kupambana na maambukizi mapya ya UVIKO 19" alisema Naibu Waziri Mwanaidi.

Aidha amesisitiza umuhimu wa kuwalinda na kuwaelekeza wazee namna ya kupata chanjo ya UVIKO 19 kutokana na umuhimu wao katika maendeleo ya taifa ndio maana Serikali kwa wamu ya kwanza ya kutoa chanjo imewapa kipaumbele.

“Nitumie nafasi hii kuwaagiza Maafisa Ustawi na Maafisa Maendeleo ya Jamii kote nchini kuhakikisha wanawahamasisha wazee kupitia majukwaa mbalimbali yakiwemo mabaraza ya wazee yaliyoko katika maeneo yao, kutumia vyombo vya habari hasa redio za kijamii ili wapate elimu kuhusu namna ya kupata chanjo hiyo katika vituo vilivyopangwa” alisema Mhe. Mwanaidi.

Wakati huo huo Naibu Waziri Mwanaidi ametumia nafasi hiyo kuwahimiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa chanjo kwa kuwa kupitia wao, elimu sahihi itawafikia wananchi kwa wakati na kuwa na uzalendo wa kuhamasisha wananchi katika suala hilo la kuchanjwa kwa hiari” alihimiza Mhe. Mwanaidi.

Aidha ,ameyahimiza Mashirika na Asasi za kiraia zinazotoa huduma kwa wazee kuandaa na kuendesha Programu mbalimbali za kuhamasisha wazee kwenda kupata chanjo ya UVIKO 19 kwa hiari yao ili kuimarisha kinga katika miili yao.

Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii Shilungu Ndaki amesema kuwa Serikali itahakikisha kundi la wazee linasimamiwa vizuri katika kupata huduma ya chanjo ya UVIKO 19 ili kulilinda kundi hilo ambalo ni muhimu kwa ustawi wa jamii.