Serikali ya Tanzania imeeleza kusikitishwa kwake na uamuzi wa Serikali ya Denmark kutangaza kuufunga ubalozi wake nchini Tanzania wakati ikibadilisha mfumo wake wa mashirikiano ili kutekeleza vipaumbele vya serikali. Nchi hiyo imesema kujipanga upya kutachangia utekelezaji wa mkakati wake mpya wa maendeleo na ushirikiano.
Waziri wa Mambo ya nje Jeppe Kofod alisema Upangaji huu upya ni kusaidia juhudi za nchi hiyo inazofanya nyumbani na duniani ili kuleta mabadiliko makubwa iwezekanavyo.
“Kipaumbele changu kama Waziri wa Mambo ya nje ni kuhakikisha usalama wa watu wa Denmark katika ulimwengu ambao demokrasia, haki za binadamu, na maadili yetu vinakandamizwa.”
Tanzania na Denmark zimekuwa na uhusiano mzuri katika miaka iliyopita. Wanasiasa wengi, maafisa wa serikali, wanasayansi, wafanyabiashara, viongozi wa dini na watendaji wa asasi za kiraia kutoka mataifa husika wameunda uhusiano wa karibu na kushiriki mazungumzo yenye tija.
Tanzania ndiyo nchi ya kwanza ya Kiafrika ambayo Denmark ilianzisha nayo ushirikiano wa kutoa misaada ya kimaendeleo mnamo 1963, muda mfupi baada ya Tanzania (wakati huo Tanganyika) kupata uhuru.