NA FARIDA SAIDY,MOROGORO.
Watu sita wanashikiliwa na jeshi la polisi Mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za kuchoma moto mali za mbalimbali za serikali ikiwemo gari aina ya Land Cruiser ,Pikipiki tatu,kifaa cha kupimia mipaka ya mashamba na kompta mpakato 3.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Fortunatus Musilim amesema tukio hilo limetokea katika kijiji cha Melela kata ya Chita Wilaya ya Kilombero,ambapo watuhumiwa walitenda kosa hilo baada ya maafisa wa Ardhi kufika katika shamba linalomilikiwa na marehemu Daud Balali ambaye alikuwa Gavana wa Banki kuu ya Tanzania.

Aidh Musilim ameongeza kuwa katika tukio hilo dereva aliyefahamika kwa jina la Damas Sanga (51 ) alijeruhiwa baada ya wananchi hao kumkukuta kwenye gari na kuanza kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kwa upande wake kamishina msaidizi wa Ardhi mkoa wa Morogoro Frank Minzikuntwe amesema vurugu hizo zimetokea baada ya maamuzi ya serikali ya kulipima shamba hilo ili liweze kupangwa upya matumizi yake baada ya kutelekezwa kwa muda mrefu huku wananchi wanalolizunguuka wakikosa maeeneo ya kulima.