Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata watuhumiwa wanaoonekana kwenye video clip mitandaoni wakiwashambulia wapenzi wakiwa kwenye faragha kwa madai ya kwamba wamewafumania.

Simbachawene ametoa agizo hilo leo Agosti 6, 2021 Jijini Dar es Salaama mara baada ya kuiona video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii ikionesha kundi la watu wakiwavamia wapenzi hao na kuwadhalilisha kwa kuwapiga na kuwarushia maneno.

“Tabia hii imeshamiri sasa kama ambavyo video nyingi zinarushwa rushwa mitandaoni, leo nitumie fursa hii kutoa msingi wa kisheria lakini kukemea tabia hii ambayo imeanza kuonekana inaota mizizi. Ni kinyume cha sheria kabisa kuwaingilia watu walio kwenye faragha.

“Wakati mwingine watu wanafanya hivyo kwa kisingizo kuwa wamefumania, hakuna fumanizi ambalo linaweza kupangwa na kikundi cha watu, wanawake na wanaume wanapanga kwenda kuwavamia na kuwaingilia uhuru wao waliopo faraghani, kitendo hicho ni kinyume cha sheria .

Amesema hata kama ni fumanizi litakuwa pale ambapo si jambo la kupangwa na huyo anayefumania awe na ndoa halali na cheti halali cha ndoa lakini sio kwa mtu ambaye ulikuwa naye tu “Huwezi kusema umemfumania hawala yako, mahusiano ya hawala ni ya kupita”.